Mcheza densi na mwalimu wa densi wa Rwanda Thierry Ishimwe, maarufu kama Titi Brown, ameanzisha mpango unaolenga kutangaza taifa la Rwanda kama eneo zuri la utalii ambao ameupa jina la ‘Rwanda in Mirror’.
Brown ameanza kampeni hiyo kwa kuzindua wimbo wenye ujumbe huo ambapo amehusisha wabunifu kadhaa wa Rwanda, akisema kwamba alimotishwa na kazi yake kama mwalimu wa densi.
“Niligundua kwamba ninaweza kuelekeza na kuchezea densi wasanii mbali mbali na watu wanapenda kwani pia inampa msanii nembo. Halafu nikafikiria kutumia mbinu hiyo hiyo kuipa nembo nchi yangu,” alisema msanii huyo.
Wimbo huo uitwao ‘Urare’unatoa mwaliko kwa watalii wa ndani kwa ndani nchini Rwanda na watu wa mataifa mengine kuzuru na kujionea Rwanda.
Brown anasifia Rwanda akisema ni nchi yenye mwonekano mzuri, yenye uongozi mzuri, amani na mapokezi mema.
Waliohusishwa katika kazi hiyo ya sanaa wanajumuisha waunda maudhui mitandaoni, waandaaji filamu na hata wanahabari ambao ni pamoja na Peace Jolis, Magna Romeo, Luna, Kenny Mirasano na Fox Makare.
Video ya Urare ina watu maarufu nchini Rwanda ambao ni pamoja na The Ben, Chriss Eazy, Papi Clever & Dorcas, Seburikoko, Mariya Yohana, Irene Murindahabi, Scovia Mutesi, Fally Merci na Luckman Nzeyimana.
Wahusika wa mpango wa Rwanda in Mirror watazuru magereza na mashule ambapo watapeleka jumbe kuhusu Rwanda na safari yake ya maendeleo.