Serikali yaunda kamati maalum ya maandalizi na kukabiliana na El Niño

Iliidhinishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne

Marion Bosire
3 Min Read
Mkutano wa Baraza la Mawaziri

Baraza la Mawaziri limeunda Kamati Maalum ya Baraza la Mawaziri ya maandalizi na kukabiliana na El Niño ili kuratibu maandalizi ya taifa.

Hatua hii inajiri kufuatia utabiri wa ujio wa mvua ya El Niño ya kiwango cha wastani hadi kikubwa inayotarajiwa kunyesha baadaye mwaka huu.

Kamati hiyo, ambayo itaongozwa na Naibu Rais Kithure Kindiki, iliidhinishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais William Ruto katika Ikulu ya Nairobi leo Jumanne.

Kwa mujibu wa taarifa ya Baraza la Mawaziri, kamati hiyo itasimamia mara moja utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Dharura wa El Niño unaolenga kupunguza athari za mvua kubwa inayotarajiwa na kulinda maisha ya wananchi, vyanzo vyao vya mapato na miundombinu muhimu.

Mpango huo unajumuisha hatua za kudhibiti mafuriko, maandalizi ya uhamishaji na makazi ya muda kwa jamii zitakazoathirika na usafishaji wa mifereji ya maji katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko.

Utahusisha pia uimarishaji wa barabara na madaraja yaliyo hatarini, pamoja na kusambaza mapema vifaa vya dharura na dawa katika maeneo muhimu.

Serikali pia itatoa ushauri kwa wakulima ili kuwasaidia kujiandaa na mabadiliko ya hali ya hewa yanayotarajiwa, huku ikianzisha hazina ya dharura itakayosaidia shughuli za misaada, urejeshaji wa hali ya kawaida na ukarabati endapo kutatokea majanga.

Hatua hiyo ni sehemu ya ajenda pana ya Baraza la Mawaziri ya kuimarisha maandalizi ya taifa dhidi ya majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi, huku ikilinda shughuli za kiuchumi na utoaji wa huduma za umma.

Kikao hicho pia kiliidhinisha sera na miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo mageuzi makubwa ya kukomesha udanganyifu katika mfumo wa mishahara serikalini, kuundwa kwa Kamati ya Kudumu ya Baraza la Mawaziri kuhusu Akili Bandia na kupitishwa kwa Sera ya Kitaifa ya Huduma za Uhamishaji wa Michakato ya Biashara (BPO) ili kuongeza fursa za ajira katika sekta ya kidijitali.

Aidha, Baraza la Mawaziri liliidhinisha fedha kwa ajili ya miradi muhimu ya miundombinu, ikiwemo awamu ya pili ya Mradi wa Kuboresha Utendaji wa Mahakama, ufadhili wa ziada wa Mradi wa Bwawa la Mwache katika Kaunti ya Kwale, pamoja na ujenzi wa barabara katika ukanda wa Isiolo–Mandera.

Katika sekta ya afya, mawaziri waliidhinisha Mfumo wa Ushirikiano wa Afya kati ya Kenya na Marekani na kuridhia Mpango wa bilioni 4.5 wa “Mother-and-Child Lifeline” utakaowezesha ujenzi wa hospitali 10 maalumu za mama na mtoto katika maeneo mbalimbali nchini.

Serikali imesema hatua hizo zinaonesha dhamira yake ya kuboresha maandalizi dhidi ya majanga, kuimarisha utoaji wa huduma za umma na kukuza uchumi endelevu kupitia mipango na uwekezaji unaoratibiwa kwa ufanisi.

Share This Article