Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kesho Julai Mosi, 2026, ataongoza maadhimisho ya miaka 30 ya kuwepo kwa mamlaka ya kukusanya mapato nchini humo, TRA.
Hafla hiyo itatumika pia kama siku ya Mlipakodi Bora ambapo walipa kodi waadilifu watatuzwa na Rais Samia anatarajiwa kukabidhi baadhi ya tuzo.
Tuzo hizo zinalenga kutambua mchango wa Walipakodi katika maendeleo ya Taifa na kuhamasisha ulipaji wa kodi kwa hiari na kwa wakati.
Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA iliasisiwa tarehe 1 Julai 1996 na tangu wakati huo mamlaka hiyo imeendelea kuimarisha ushirikiano na Walipakodi.
Imeendelea pia kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali na kuchangia maendeleo ya sekta mbalimbali kupitia fedha zinazotokana na kodi.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya kesho ni, “Miaka 30 ya TRA, Kulipa Kodi ni Uzalendo na Ushujaa kwa Maendeleo na Kujitegemea kwa Taifa Letu,”.
TRA imewapongeza na kuwashukuru Walipakodi wote kwa kuendelea kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati, huku ikisisitiza kuwa kodi ndiyo nguzo muhimu ya maendeleo na ustawi wa taifa hilo la Afrika Mashariki.