Mikusanyiko ya umma DRC yapigwa marufuku kufuatia Ebola

Mikusanyiko ya umma imepigwa marufuku katika majimbo ya Kinshasa, Tshopo, Bas Uele na Haut Uele.

Martin Mwanje
1 Min Read
Picha kwa hisani ya ICRC

Mikusanyiko ya umma imepigwa marufuku katika majimbo manne yaliyo katika hatari kubwa zaidi ya kukumbwa na maambukizi ya ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC. 

Majimbo hayo yanajumuisha Kinshasa, Tshopo, Bas Uele na Haut Uele.

Mamlaka za nchi hiyo zinasema hatua hiyo inajumuisha kusitishwa kwa mikutano, mikusanyiko ya watu wengi na maandamano.

Aidha, mamlaka hizo zinasema hatua hiyo inalenga kuimarisha udhibiti wa ugonjwa huo nchini humo, zikihofia msambao zaidi wa Ebola ikiwa hatua madhubuti hazitachukuliwa.

Madaktari 17  ni miongoni mwa watu zaidi ya 200 ambao wamefariki kutokana na ugonjwa wa Ebola nchini DRC.

Shirika la Afya Duniani, WHO limesema wahudumu wengine 75 wa afya wameambukizwa virusi vya ugonjwa huo tangu nchi hiyo ilipotangaza kuzuka kwa ugonjwa Mei 25 mwaka huu.

Wizara ya Afya nchini DRC imeripoti visa 875 vya maambukizi ya Ebola pamoja na vifo 202.

Imedokeza kuwa watu 67 wamepona ugonjwa huo huku wagonjwa 379 wakilazwa katika sehemu za kuwatibu wagonjwa wa Ebola.

Share This Article