Brazil na Ujerumani zalenga kufuzu kwa raundi ya 16 Jumatatu

Brazil waliongoza kundi C kwa alama saba wakitoka sare ya 1-1 na Morocco kabla ya kuwapiga Haiti na Scotland magoli 3-0 kila moja.

Dismas Otuke
2 Min Read

Mabingwa wa Dunia mara tano Brazil na mabingwa mara nne Ujerumani watashuka uwanjani Jumatatu usiku katika siku ya pili ya mechi za raundi ya 32 za Kombe la Dunia wakilenga kusonga mbele.

Vijana wa Samba wanaonolewa makali na Carlo Ancelotti watafungua ratiba ya siku dhidi ya Blue Samurai ya Japani uwanjani Houston, Marekani kuanzia saa mbili usiku wa Jumatatu.

Itakuwa ni mara ya tisa kwa timu hizo kukutana, Brazil wakashinda tatu huku Japani wakiibuka kidedea mechi moja, nayo michuano mitatu ikamalizikia sare.

Brazil waliongoza kundi C kwa alama saba, wakitoka sare ya 1-1 na Morocco kabla ya kuwapiga Haiti na Scotland magoli 3-0 kila moja.

Japani nao walichukua nafasi ya pili kundini F kwa pointi 5, wakitoka sare ya 2-2 na Uholanzi, wakaikung’uta Tunisia 4-0 na kuambulia sare ya 1-1 na Uswidi.

Baadaye saa tano unusu, itakuwa zamu ya Ujerumani kukabiliana na Paraguay ugani Boston, Marekani katika mechi inayotarajiwa kuegemea upande mmoja.

Ujerumani waliongoza kundi E kwa alama 6, wakiwashinda Curacao 7-1 na Ivory Coast 2-1 kabla ya kupigwa na Ecuador 2-1.

Paraguay ilifuzu ikiwa mojawapo wa timu bora za nafasi ya tatu ikizoa alama 4 kwa kuishinda Uturuki goli moja bila jawabu, na ikashindwa na Marekani magoli 2-0 na hatimaye kutoka sare kappa na Australia katika kundi D.

Itakuwa mechi ya tatu kati ya Ujerumani na Paraguay, Ujerumani wakiwashinda Paraguay 1-0 katika Kombe la Dunia mwaka 2002 kabla ya kwenda sare ya 3-3 katika mchuano wa kirafiki mwaka 2013.

 

Share This Article