Washukiwa 8 wa mkasa wa moto Utumishi Girls kufanyiwa uchunguzi wa kiakili

Uchunguzi huo utafanywa katika Hospitali ya Akili ya Mathare Juni 29 kabla ya kutajwa tena kwa kesi dhidi ya washukiwa Julai 1 mwaka huu.

Martin Mwanje
2 Min Read
Wanafunzi wanaoshukiwa kusababisha mkasa wa moto Utumishi Girls Academy walipofikiwa mahakamani awali

Mahakama Kuu ya Kibera imeagiza wanafunzi 8 wanaoshukiwa kusababisha mkasa wa moto katika shule ya Utumishi Girls Academy mjini Gilgil, kaunti ya Nakuru mwishoni mwa mwezi Mei kufanyiwa uchunguzi wa kiakili. 

Wanafunzi hao watafanyiwa uchunguzi huo na daktari wa akili ya watoto Juni 29 mwaka huu katika Hospitali ya Akili ya Mathare.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Msajili wa mahakama hiyo Barbara Akinyi wakati washukiwa walipofika mbele yake kwa njia ya mtandao.

Kesi dhidi ya washukiwa ilitajwa mara ya kwanza leo Ijumaa.

Akinyi aliagiza matokeo ya uchunguzi huo kuwasilishwa kwa mahakama kabla ya kutajwa tena kwa kesi hiyo.

Kadhalika, mahakama iliagiza washukiwa kufanyiwa uchunguzi na afisa wa watoto katika makazi ya watoto ya Kabete leo Ijumaa. Ikiwa uchunguzi huo hautamalizika leo, mahakama iliagiza ufanywe hadi mwishoni mwa wiki hii na ripoti kuwasilishwa kabla ya kutajwa tena kwa kesi hiyo.

Wakati wa kutajwa kwa kesi hiyo, upande wa mashtaka ukiongozwa na Naibu Mkurugenzi Mwandamizi wa Mashtaka ya Umma Vincent Monda uliwasilisha maombi kadhaa ikiwa ni pamoja na washukiwa kuwakilishwa na mawakili wa kujitolea.

Lengo ni kuhakikisha kesi hiyo inamalizika ndani ya muda unaotakikana kwa mujibu wa sheria ya watoto.

Kesi dhidi ya wanafunzi hao itatajwa tena mbele ya Jaji Diana Kavedza Julai 1, 2026.

Upande wa mashtaka uliiomba mahakama kuwa washukiwa waendelee kuzuiliwa katika makazi ya watoto ya Kabete wakati wakisubiri maelekezo zaidi kutoka kwake.

Wanafunzi 16 walifariki wakati mkasa wa moto ulipotokea katika shule ya Utumishi Girls Academy Mei 28 huku wanafunzi wengine 79 wakijeruhiwa.

Uchunguzi ulibaini bweni la shule hiyo lilitetekezwa kimakusudi na kusababisha maafa hayo.

Serikali imeapa kuwachukulia hatua kali wanafunzi watakaopatikana wakijiusisha katika uovu kama huo siku zijazo.

 

 

Share This Article