Washukiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarti wamekamatwa kwenye operesheni ya kijasusi iliyotekelezwa katika kaunti ya Kilifi.
Kwenye operesheni hiyo iliyoendeshwa katika eneo la Sakina, Huduma ya Taifa ya Polisi ilisema wawili hao walikuwa wakihusika na biashara haramu ya ulanguzi wa bangi.
Maafisa hao wa polisi walipata nusu gunia ya bangi, mbegu za bangi, mifuko kadhaa iliyokuwa imepakiwa bangi tayari kwa usambazaji, kifaa cha kidijitali cha kupima uzani, nyundo, na fedha zinazoaminika zilitokana na uuzaji wa bangi, miongoni mwa ushahidi mwingine.
Washukiwa hao wanazuiliwa kwenye korokoro za polisi, huku uchunguzi ukiendelea kabla ya kufikishwa mahakamani.
Kulingana na Huduma ya Taifa ya Polisi, operesheni hiyo ni sehemu ya juhudi zinazoendelea za kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati kote nchini Kenya.
Wananchi wamehimizwa kutoa habari kwa maafisa wa usalama, kuhusu biashara wanazotilia shaka ili kufanikisha vita dhidi ya utumizi na ulanguzi wa mihadarati.