Kenya inajiunga na ulimwengu leo Ijumaa kuadhimisha Siku ya Kimataifa dhidi ya Matumizi na Ulanguzi wa Dawa za Kulevya (IDADA).
Humu nchini, maadhimisho hayo yataandaliwa katika Kituo cha Matibabu na Urekebishaji Tabia cha Miritini, kaunti ya Mombasa, kinachosimamiwa na Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Mihadarati (NACADA).
Washiriki watajadili kuhusu sera za kitaifa za kudhibiti dawa za kulevya, uhamasishaji wa umma kuhusu aina mpya za dawa za kulevya, na kuonyesha ubunifu kwenye mbinu za urekebishaji tabia zinazofanyiwa majaribio katika kituo cha Miritini.
Maadhimisho hayo yananyika wakati ambapo Kenya imeimarisha vita dhidi ya utumizi na ulanguzi wa dawa za kulevya hususan miongoni mwa vijana.
NACADA imesema maadhimisho hayo yatatoa fursa kwa serikali kukariri kujitolea kwake kujumuisha upatikanaji wa matibabu bila vikwzo kupitia huduma zilizopanuliwa katika kituo cha Miritini.
Kulingana na NACADA, hatua zinazochukuliwa sasa pamoja na mbinu bunifu zitasaidia kukabiliana na tatizo la matumizi na ulanguzi wa dawa za kulevya kote duniani.