Jaji Mkuu Koome ataka wanasiasa wanaofadhili uhuni kuwajibishwa

Wahuni wameibuka kuwa kero nchini huku wanasiasa wakilaumiwa kwa kuwatumia vijana kusababisha vurugu wakati wa mikutano katika maeneo mbalimbali nchini.

Martin Mwanje
2 Min Read
Jaji Mkuu Martha Koome

Jaji Mkuu Martha Koome ametoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwachukulia hatua kali wanasiasa wanaotumia magenge ya wahuni kuzua vurugu wakati wa mikutano nchini. 

Jaji Koome ameitaka IEBC kuwawajibisha wanasiasa kama hao kwa mujibu wa kanuni ya maadili mema.

Amelaani hulka ya wanasiasa kutumia wahuni kusababisha vurugu wakati wa kipindi cha kampeni kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2027.

“Wanasiasa wachache hawapaswi kuwashika mateka mamilioni ya Wakenya,” alilalama Jaji Mkuu Koome wakati akishutumu vikali mwenendo huo.

Aliyasema hayo hii leo Jumatano wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mpango wa Kimkakati wa IEBC wa mwaka 2024–2029 iliyofanyika jijini Nairobi.

Aidha, wakati wa hafla hiyo, Mpango wa Kusimamia Uchaguzi wa mwaka 2025-2027 pia ulizinduliwa.

Matamshi ya Jaji Koome yanakuja wakati ambapo wahuni wameibuka kuwa kero nchini, mara nyingi wakionekana kuvuruga mikutano katika maeneo mbalimbali na kisha kwenda mafichoni.

Kwa mfano, siku chache zilizopita, wahuni  walivuruga mkutano wa kujadili bajeti ulioandaliwa katika kanisa la All Saints Cathedral jijini Nairobi.

Uchunguzi wa kubaini waliohusika katika uhuni huo unaendelea huku watu kadhaa wakiwa wamekamatwa.

Hali imekuwa vivyo katika maeneo mbalimbali nchini hasa wakati wa mikutano ya kisiasa huku kukiwa na madai ya wahuni hao kufadhiliwa na wanasiasa.

Kongamano la Maaskofu wa Kanisa Katoliki nchini (KCCB) pia limeelezea wasiwasi  wake kuhusu kuibuka tena kwa makundi ya wahuni, likionya kuwa utumizi wa ghasia kuvuruga mikutano unahujumu haki ya kidemokrasia.

Share This Article