Mwanahabari wa Shirika la Utangazaji Nchini Kenya (KBC) Millicent Kubai, ndiye mshindi wa makala ya kwanza ya tuzo za wanahabari wanaosimulia hadithi kuhusu ugonjwa wa UKIMWI (HIV & STIs Reporting Media Awards),tuzo zinazoandaliwa na shirika la kimataifa la AHF Kenya.
Makala ya Redio yaliyoandaliwa na Kubai kwa kichwa ‘Life Beyond the Diagnosis’ ukipenda maisha baada ya vipimo, yalimwezesha kuwapiga wengine kumbo na kuibuka mshindi wa tuzo kuu iliyoambatana na donge nono la shilingi nusu milioni, kando na kutawazwa mshindi wa kitengo cha makala bora ya redio.

“Nimefurahia kuibuka mshindi;wajua kuwa kuibuka mshindi kati ya washindani 99 sio kazi lelemama .Mwanzo nilishukuru shirika la KBC, kwa kunipa jukwaa la kuangazia sauti yangu kuhusu masaibu yanayowasibu Wakenya wanaoishi na virusi vya Ukimwi.Nitaekeza kiasi cha hela hizi na nyingine nitumie kutayarisha makala zaidi.”alisema Kubai
‘Life beyond the diagnosis’ ni makala ya redio yanayosimulia jinsi mtu anapaswa kukabiliana na uhalisia wa maisha baada ya kupatikana kuwa na virusi vya HIV, pamoja na kupambana na unyanyapaa unaoambatana na hali hiyo.
“Niliandaa makala ya Life beyond diagnosis, ili kuangazia wanayopitia watu baada ya kutembelea vituo vya kupimwa na kutoa ushauri nasaha (VCT), na kuthibitishwa kuwa na virusi vya HIV,huku idadi kubwa wakihepa vipimo kwa kuhofia unyanyapaa,” alisema Kubai.
“Aidha, nilibaini kuwa wanawake wengi hutembelea vituo vya VCT ,ikilinganishwa na wanaume ambao wanahepa kupimwa na badala yake kuendelea kusambaza virusi.”aliongeza mtangazaji huyo.
Makala hayo yalichaguliwa bora baada ya kuzoa alama 117.9 kati ya 140, huku washindi wakitawazwa katika vitengo saba tofauti vya magezeti, Redio, Runinga na mitandaoni.
Tuzo hiyo inalenga kuwatambua na kuwatuza Wanahabari wanaotekeleza jukumu muhimu la kuhamasisha umma kuhusu ugongwa wa Ukimwi.