Kenya yaondolewa kwenye vikwazo vya usafiri vilivyotolewa na Israel

Tom Mathinji
1 Min Read
Katibu katika Wizara ya Mambo ya Nje Korir Sing'Oei.

Ni afueni kwa Kenya baada kuondolewa kwenye orodha ya vikwazo vya usafiri, iliyotolewa na Israel kutokana na chamko la ugonjwa wa Ebola.

Hatua hiyo imejiri saa chache baada ya Wizara ya Kenya ya Mambo ya Nje kulalamikia vikali hatua hiyo, iliyoitaja kuwa isiyofaa.

Kwenye ukurasa wa X, Ubalozi wa Israel nchini Kenya, ulisema umeamua kuondoa Kenya na Rwanda kwenye orodha ya mataifa yaliyowekewa vikwazo vya usafiri kutoka na chamko la ugonjwa wa Ebola.

“Tunafahari kutangaza kuwa Wizara ya  Afya ya Israel imeamua kuiondoa Kenya na Rwanda kutoka kwa orodha ya nchi ambazo zimewekewa vikwazo vya usafiri  kuhusiana na chamko la Ebola,” ulisema Ubalozi wa Israel nchini Kenya.

Katibu wa Wizara ya Mambo ya Nje Korir Sing’Oei, amekaribisha hatua hiyo ya Israel, akisema kuwa hivyo ndivyo marafiki huchukua hatua.

“Tunakaribisha kikamilifu hatua ya Israel ya kuondoa Kenya kwenye orodha ya vikwazo vya usafiri iliyotolewa na Israel kuhusiana na chamko la ugonjwa wa Ebola,” alisema Sing’Oei.

Ugonjwa wa Ebola ulizuka katika eneo la Ituri, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku ukienea hadi nchini Uganda.

Kenya inalenga kujenga kituo cha karantini katika kaunti ya Laikipia, kuwashughulikia raia wa Marekani ambao wataugua ugonjwa huo.

Share This Article