Sakaja amsimamisha kazi Analo, afanyia mabadiliko usimamizi wa Nairobi

Tom Mathinji
1 Min Read
Gavana wa Nairobi Johnson sakaja.

Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja, amemsimamisha kazi Patrick Analo Akivaga, siku moja baada ya maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi EACC, kumkamata kwa madai ya kushiriki ufisadi.

Analo alikamatwa akiwa na shilingi milioni 65,300,000 nyumbani kwake Syokimau kaunti ya Machakos, baada ya maafisa hao kutekeleza operesheni hiyo.

Huku akimtimua Analo kwenye wadhifa wa Afisa Mkuu wa mipango ya Ustawishaji wa miji, Sakaja amemteua Dominic Mutegi kuchukua wadhifa huo, huku akiwaonya maafisa wa serikali ya kaunti kuwa watawajibikia majukumu yao binafsi.

Aidha Gavana huyo pia amemteua Ibrahim Auma Nyangoya kuwa Afisa Mkuu wa Fedha na mipango ya kiuchumi, kuchukua mahala pa Charles Kerich anayekabiliwa na kesi.

Gavana Sakaja alisema kuwa serikali ya kaunti ya Nairobi, itashirikiana na wachunguzi wa EACC kwenye kesi dhidi ya Analo.

“Serikali ya kaunti ya Nairobi inaheshimu uzingatiaji wa sheria na itashirikiana na wachunguzi wa EACC na asasi zingine kwenye uchunguzi unaoendelea,” alisema Sakaja kupitia kwa taarifa.

Kwa sasa utayarishaji wote  wa kuidhinisha mipango ya ustawi umesitishwa, hadi kamati ya kiufundi itakapobuniwa upya kikamilifu.

Kaunti ya Nairobi imewahimiza wakazi wawe na subira huku uchunguzi ukiendelea, ikiwahakikishia  kuwa  utoaji huduma hautahujumiwa.

Share This Article