Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi ametoa wito kwa mataifa ya Afrika kupiga kumbo utegemeaji wa misaada, badala yake yakumbatie biashara, uwekezaji na uongezaji bidhaa thamani, huku bara hilo linapoimarisha ushurikiano wa kiuchumi na Korea Kusini.
Akizungumza kwenye mkutano unaoendelea kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Afrika na wale wa Korea Kusini Jijini Seoul, Mudavadi alisema Afrika ni sharti ikumbatie ushirikiano wa kimkakati ili kuafikia maendeleo endelevu na ubunifu wa nafasi za ajira.
Akihutubia mawaziri hao pamoja na maafisa wa ngazi za juu kutoka Afrika na Korea Kusini, Mudavadi ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, alitaja mkutano huo kuwa jukwaa muhimu katika kuimarisha ushirikiano na kupiga jeki ufanisi wa pamoja, wakati huu ambapo kuna changamoto za kiuchumi na kisiasa.
“Mkutano wetu unafanyika wakati ambapo tunashuhudia changamoto za kisiasa na kuvurugwa kwa uchumi na maendeleo,” alisema Mudavadi.
Alisisitiza kuwa ushirikiano wa Afrika na Korea Kusini unapaswa kujikita kwenye biashara na uwekezaji badala ya kutegemea misaada, akidokeza kuwa ushirikiano bora na sekta za kibinafsi utafanikisha ukuaji wa viwanda, hatua itakayosababisha upatikanaji wa nafasi za ajira kwa idadi ya watu inayozidi kuongezeka Afrika.