Serikali yasema inageuza sekta ya mifugo kaskazini mwa nchi

Martin Mwanje
1 Min Read
Picha kwa hisani ya World Vision International

Serikali ya Kenya Kwanza inasema inaifanyia mageuzi sekta ya mifugo kaskazini mwa nchi ili kuhakikisha wakazi wanapata mapato yatakayobadilisha dira ya maisha yao. 

“Kupitia moja ya mipango mikubwa zaidi ya uongezaji tena idadi ya mifugo katika miaka ya hivi karibuni, tumetoa zaidi ya kondoo, mbuzi na ng’ombe kwa zaidi ya kaya 10,000 katika kaunti zote kame 16, na kusaidia familia kujenga upya utajiri wa mifugo waliofariki kutokana na kiangazi na changamoto zingine,” alisema Rais Ruto wakati wa sherehe za Sikukuu ya Madaraka leo Jumatatu.

Ili kuimarisha mapato ya wafugaji, Ruto amesema serikali iumetoa chanjo kwa zaidi ya mifugo milioni 10, na kupanua uzalishaji wa chanjo nchini hadi zaidi ya dozi milioni 123 mbali na kuanzisha maeneo ya kulisha mifugo na vituo vya kuhifadhi malisho.

Alidokeza kuwa maafisa wa kilimo 2,000 pia watatumwa katika maeneo kame kutoa ushauri kwa wakulima na kuwaunganisha na masoko ili kuongeza mapato yao.

“Matokeo ya hatua hizi za kimakusudi tayari yameanza kuonekana. Nyama inayouzwa nje ya nchi imeongezeka kwa asilimia 84, kutoka shilingi bilioni 8.9 mwaka 2022 hadi bilioni 16.4 mwaka 2025,” aliongeza Ruto.

 

Share This Article