Raia wa Ethiopia leo Jumatatu Juni 1, 2026, wanashiriki Uchaguzi Mkuu kuwachagua wabunge, huku Waziri Mkuu Abiy Ahmed akijizatiti kuendeleza utawala wake katika taifa hilo la upembe wa Afrika.
Huu ni Uchaguzi Mkuu wa saba nchini humo, tangu kukamilika kwa uongozi wa kijeshi, na ambao umetajwa kuwa muhimu kwenye safari ya kidemokrasia ya taifa hilo.
Vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa kumi na mbili asubuhi saa za taifa hilo, ambapo maelfu ya watu tayari walikuwa wamepanga foleni kutekeleza haki zao za kikatiba.
Kwenye uchaguzi huo, wananchi wanawachagua wabunge 547, huku chama kitakachopata viti 274, kikipata fursa ya kubuni serikali ijayo na kuongoza taifa hilo miaka mitano ijayo.
Aidha, uchgauzi huo hautafanyika katika eneo la Tigray, ambako tume ya uchaguzi nchini humo imesema kuna hali isiyofaa kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyoanza mwaka 2020 na kukomeshwa mwaka 2022.