Timu ya taifa ya soka ya Kenya kwa wanawake chini ya umri wa miaka 17, itachuana na wenzao wa Uganda katika mkondo wa kwanza wa raundi ya pili kufuzu kwa Kombe la Dunia leo Ijumaa jioni jijini Kampala.
Junior Starlets, wanaowania kucheza Kombe la Dunia kwa mara ya pili, walifuzu kwa raundi ya pili baada ya kuibandua Namibia, wakati Uganda wakiitema Zimbabwe katika raundi ya kwanza.
Mkondo wa pili utachezwa Nairobi wiki ijayo huku mshindi akiingia raundi ya tatu na ya mwisho.
Fainali za Kombe la Dunia zitaandaliwa nchini Morocco baina ya Oktoba 17 na Novemba 7 mwaka huu.