Bei ya dizeli kupunguzwa kwa shilingi 10 zaidi

Shilingi hizo zitapunguzwa kwa kipindi cha kati ya Juni 15 na Julai 14, 2026 EPRA itakapotangaza bei mpya za mafuta nchini mwezi ujao.

Martin Mwanje
2 Min Read

Bei ya dizeli itapunguzwa kwa shilingi 10 zaidi wakati bei mpya za mafuta zitakapotangazwa mwezi ujao na Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli, EPRA kwa kipindi cha kati ya Juni 15 na Julai 14. 

Tangazo hilo limetolewa na Rais William Ruto wakati akihutubia taifa katika Ikulu ya Mombasa leo Ijumaa.

“Nimeagiza kwamba katika kipindi kijacho cha kutangaza bei mpya za mafuta, serikali itapunguza bei ya dizeli kwa shilingi 10 zaidi kwa kipindi cha mwezi Juni hadi Julai,” alisema Rais Ruto aliyekuwa ameandamana na wadau wa sekta ya uchukuzi wa umma.

“Hatua hii inalenga kudhibiti bei za mafuta na kutoa afueni zaidi kwa watumiaji.”

Huku Wakenya wakilalamikia bei za juu za mafuta, Ruto amesema ukweli ni kwamba nchi hii inahisi athari za janga linaloikabili dunia nzima.

“Ukweli ni kwamba Kenya inakabiliwa na athari za janga lililosababishwa na mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati, na siyo tatizo linaloikabili Kenya pekee,” aliongeza kiongozi wa nchi akionya dhidi ya kuingiza siasa kwa suala hilo.

Amewahakikishia Wakenya kuwa serikali imechukua hatua za kuwakinga dhidi ya athari za janga hilo, akisema kipindi cha miezi miwili iliyopita, serikali imetumia shilingi  bilioni 13.7 kudhibiti hali hiyo.

Mapema wiki hii, EPRA ilipunguza bei ya mafuta ya dizeli kwa shilingi 10.06 kwa lita huku ikiongeza bei ya mafuta taa kwa shilingi 38.60 kwa kila lita.

Kupitia kwa taarifa Jumatatu jioni, EPRA ilisema bei hizo mpya zitatekelezwa kuanzia Jumanne wiki hii, Mei 19, 2026 hadi Juni 14, 2026.

Kufuatia mabadiliko hayo, lita moja ya mafuta ya super petrol jijini Nairobi inauzwa kwa shilingi 214.25, dizeli shilingi 232.86 na mafuta taa shilingi 191.38.

 

Share This Article