Maafisa wa polisi wamemkamata mshukiwa wa mauaji ya mwalimu katika kaunti ya Kirinyaga mwezi Machi mwaka huu.
Peter Kanumbi alikamatwa akiwa kwenye maficho yake eneo la Mpeketoni, kaunti ya Lamu, baada ya miezi kadhaa ya msako dhidi yake.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imesema Kanumbi alitoroka Kirinyaga baada ya kutekeleza mauaji ya mwalimu Betty Wanjiru Nyaga eneo la Mwea Mashariki Machi 12, 2026.
“Maafisa wa polisi walimtafuta mshukiwa huyo na kumpata katika eneo la Mpeketoni, kaunti ya Lamu, walimkamata kabla avuke mpaka kuingia nchi jirani ya Somalia kwa lengo la kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria,” ilisema DCI.
Baada ya kukamatwa, Kanumbi alirejeshwa kaunti ya Kirinyaga na kufikishwa kwenye mahakama ya Kirinyaga, huku polisi wakipewa siku tano kumzuilia kutoa fursa ya uchunguzi zaidi kufanywa.