Maafisa wa kukabiliana na ulanguzi wa mihadarati (ANU) katika kaunti ya Kilifi, wamewakamata washukiwa wawili wa ulanguzi wa mihadarati kwenye operesheni iliyotekelezwa katika eneo hilo.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinani (DCI), imesema wawili hao Eisha Mzungu Kalama na mshirika wake Jamal Chilumo Chiraga, walipatikana na bangi yenye thamani ya shilingi milioni 4.2 kwenye nyumba yao katika mtaa wa Kisumu ndogo.
“Wakati wa operesheni hiyo, maafisa hao walifanya msako kwenye nyumba ya washukiwa hao na kupata magunia mawili na nusu ya bangi yenye uzani wa kilo 142, yakiwa tayari kusambazwa,” ilisema DCI kupitia ukurasa wa X.
Washukiwa hao wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Kilifi, wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Mihadarati hiyo pia inazuiliwa na itatumika kama ushahidi huku uchunguzi ukiendelea kuhusu mitandao ya ulanguzi wa mihdarati katika eneo hilo.