Kenya yaimarisha hatua za uangalizi wa Ebola mpakani Busia

Nchi jirani ya Uganda imethibitisha visa viwili vya Ebola kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

radiotaifa
2 Min Read
Maafisa wakikabiliana na ugonjwa wa Ebola / Picha ya awali kwa hisani ya IFRC

Serikali kuu nchini Kenya kwa kushirikiana na serikali ya kaunti ya Busia zimeimarisha hatua za uangalizi wa ugonjwa wa Ebola kwenye mpaka kati ya Kenya na Uganda. 

Hii ni kufuatia mlipuko wa ugonjwa huo katika Jamhuri ya Demokrasia ya Congo, DRC.

Visa viwili vya ugonjwa huo pia vimethibitishwa katika nchi jirani ya Uganda.

Akizungumza kwenye ofisi ya afya ya umma kwenye mpaka wa Busia, Naibu Gavana wa kaunti ya Busia Arthur Odera amesema mamlaka zimeimarisha hatua za vipimo na ufuatiliaji kuhakikisha watu wote wanaovuka mpaka hawana maambukizi ya Ebola.

Odera, ambaye pia anahudumu kama Waziri wa Afya wa kaunti hiyo amesema serikali ya kaunti inafanya kazi kwa karibu na Shirika la Msalaba Mwekundu kuimarisha vipimo katika maeneo yote ya kuingia na kutoka yaliyopo kwenye mpaka kati ya Kenya na Uganda.

Amedokeza kuwa maafisa wa afya ya umma wamepelekwa kupima halijoto na kampeni za hamasisho miongoni mwa wasafiri.

Hayo yanajiri wakati ambapo mamlaka nchini Uganda zimefutilia mbali hofu ya kuenea kwa ugonjwa wa ebola nchini humo ikisema nchi hiyo iko salama kutembelewa wakati wowote.

Kwenye taairifa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Bodi ya Utalii ya nchi hiyo (UTB) Juliana Kagwa amesema licha ya visa viwili vya ugonjwa huo kuripotiwa nchini humo, hakuna haja ya kuhofu.

“Uganda imeripoti visa viwili kutoka nje ya nchi hiyo vinavyohusisha raia wa Congo walioingia Uganda kutokea DRC. Kwa bahati mbaya, mgonjwa mmoja alifariki na amerejeshwa nchini mwake, huku wa pili akiendelea kutibiwa chini ya uangalizi wa Wizara ya Afya,” alisema Kagwa.

“Muhimu zaidi, kuna maambukizi SIFURI kwa sasa ndani ya nchi au maambukizi katika jamii ndani ya Uganda. Wizara ya Afya ya Uganda inaendelea kufanya uangalizi mkali, kufanya vipimo, ufuatiliaji, na uitikiaji wa haraka nchini kote.”

Afisa huyo amesema Uganda ina tajiriba ya kudhibiti milipuko ya ugonjwa wa ebola na magonjwa mengine ya milipuko, na kwa misingi hiyo, shughuli zingine kama vile utalii na huduma za usafiri zinaendelea kama kawaida.

Taarifa ya Martin Mwanje na Sayyid Abdalla

 

Share This Article