Wasafiri walioamka asubuhi na mapema leo Jumatatu kwa shughuli zao za kawaida walipigwa na butwaa, kufuatia mgomo wa kitaifa wa wahudumu wa magari ya usafiri wa umma kupinga kuongezwa kwa bei ya mafuta.
Vituo vingi vya magari kote nchini vilibaki mahame, vingine vikiwa maegesho ya magari ya usafiri wa umma.
Aidha, wananchi wengi waliopanga kusafiri kuelekea kazini wamelazimika kurejea nyumbani kutokana na kukosa magari ya usafiri.
Maandamano pia yameshuhudiwa katika maeneo kadhaa ya nchi, huku barabara zikifungwa kwa mawe na waandamanaji kuteketeza magurudumu.
Wenye magari ya usafiri wa umma walitangaza kuanza kwa mgomo kote nchini hii leo kupinga hatua ya serikali kuongeza bei ya mafuta.
Siku nne zilizopita, Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Petroli (EPRA) ilitangaza nyongeza ya bei ya bidhaa za mafuta iliyoanza kutekelezwa Mei 15 hadi Juni 14, 2026.
Kulingana na bei hizo mpya, lita moja ya mafuta ya petroli iliongezwa kwa shilingi 16.65, dizeli ikapanda kwa shilingi 46.29, kwa lita, huku bei ya mafuta taa ikikosa kubadilika.
Jijini Nairobi, lita moja ya mafuta ya mafuta ya petroli inauzwa kwa shilingi 214.25, dizeli shilingi 242.92, huku lita moja ya mafuta taa ikiuzwa kwa shilingi 152.78.
Kulingana na EPRA, bei hiyo mpya inajumuisha ushuru husika.
Serikali imetangaza ruzuku kupitia Hazina ya Maendeleo ya Petroli, ikilenga kutumia shilingi bilioni 5 ili kuwakinga Wakenya dhidi ya bei za juu za dizeli na mafuta taa.