Kindiki atetea uuzaji wa hisa za serikali kwenye mashirika

Amesema hatua hiyo itaipunguzia serikali mzigo wa kukopa madeni au kuongeza kodi ili kupata fedha za kufadhili miradi hiyo. 

radiotaifa
2 Min Read

Naibu Rais Prof. Kithure Kindiki ametetea uuzaji wa hisa za serikali kwenye mashirika yaliyoorodheshwa kwa soko la hisa kwa lengo la kukusanya fedha za kufadhili miradi mikubwa ya miundombonu nchini.

Amesema hatua hiyo itaipunguzia serikali mzigo wa kukopa madeni au kuongeza kodi ili kupata fedha za kufadhili miradi hiyo.

Prof. Kindiki alipongeza uanzishwaji wa Mfuko wa Kitaifa wa Miundombinu, NIF aliyosema ni njia bunifu ya serikali kufadhili miradi mikubwa bila ya kuwarundikia walipaji ushuru madeni zaidi.

“Sasa tuna njia ya kukusanya fedha zaidi ndani ya nchi bila kuongeza madeni au kodi. Tunakusanya fedha kiubunifu kwa kuweka pamoja rasilimali za kufadhili miradi,” alisema Naibu Rais.

Aliongeza kuwa NIF tayari imepokea shilingi bilioni 100 kutokana na mauzo ya hisa katika kampuni ya Kenya Pipeline na shilingi bilioni 245 kutokana na mauzo ya hisa kwenye kampuni ya Safaricom.

“Mfuko wa Miundombinu umeleta mabadiliko kwa sababu kwa kila shilingi tunayowekeza kwenye mfuko huo, tutapata shilingi zingine 10. Tunakaribia tamati ya utekelezaji wake kwa sababu sheria imewekwa na sasa tuna fedha za kutekeleza miradi,” alisema Prof. Kindiki.

Aliyasema hayo leo Ijumaa katika ofisi yake iliyoko katika jumba la Harambee House Annex jijini Nairobi alipopokea ripoti za hali ya miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa nchini kote.

Naibu Rais aliarifiwa juu ya hali ya miradi hiyo na Waziri wa Maji Eric Mugaa na maafisa wengine waandamizi wa wizara hiyo.

Taarifa ya DPCS

Share This Article