Wizara ya Afya ya Kenya imechukua tahadhari kutokana na kuzuka upya kwa ugonjwa wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Afrika CDC), kilitngaza kuzuka upya kwa Ebola katika wilaya ya Ituri Mashariki mwa DRC, maeneo yaliyoathiriwa zaidi yakiwa Mongwalu na Rwampara ambayo ni maarufu kwa uchimbaji madini ya dhahabu.
Kupitia kwa taarifa siku ya Jumamosi, Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini Kenya Dkt. Patrick Amoth, amesema hadi sasa Kenya haijanakili kisa chochote cha Ebola.
Dkt. Amoth alisema Wizara ya Afya imebuni kundi la kushughulikia ugonjwa wa Ebola pamoja na kuweka katika hali ya tahadhari kituo cha kitaifa cha kushughulikia dharura, kwa uangalizi na ushirikishi.
Amoth ametoa wito kwa umma kuzingatia habari kutoka kwa Wizara ya Afya na Taasisi za kimataifa, na kuepuka kusambaza habari ambazo zinaweza sababisha taharuki.
Maafisa nchini Uganda pia wamethibitisha kisa kimoja cha Ebola, wakisema mwanamume mwenye umri wa miaka 59 aliyefariki siku ya Alhamisi, aligunduliwa kuugua ugonjwa huo.