Ayub Njoroge Gitau ateuliwa chansela chuo kikuu cha Nairobi

Aliteuliwa katika kikao maalum cha baraza la chuo hicho, kilichofanyika Alhamisi, Mei 14, 2026.

Marion Bosire
2 Min Read

Chuo kikuu cha Nairobi kimemteua rasmi Ayub Njoroge Gitau kuwa Naibu Chansela wake mpya, baada ya mvutano wa muda mrefu uliodumu kwa miaka kadhaa.

Uteuzi wake unafuatia kikao maalum cha baraza la chuo kilichofanyika Alhamisi, Mei 14, 2026, kujadili mabadiliko ya uongozi katika taasisi hiyo.

Katika taarifa, baraza la chuo lilitangaza kuwa limemuidhinisha Gitau kuwa Naibu Chansela wa 9 wa Chuo Kikuu cha Nairobi baada ya saa kadhaa za majadiliano.

Baraza hilo lilisema kuwa uteuzi huo unalenga kuanzisha enzi mpya kwa taasisi hiyo huku ikijitahidi kuimarisha uongozi, ubora wa taaluma na maendeleo ya taasisi.

“Baraza la Chuo Kikuu cha Nairobi, kufuatia mashauriano katika kikao maalum kilichofanyika Alhamisi, Mei 14, 2026, limetangaza uteuzi muhimu wa viongozi utakaoanzisha enzi mpya kwa taasisi hiyo,” baraza lilitangaza.

Mbali na uteuzi wa Gitau, baraza la chuo pia lilimuidhinisha Josiah Omollo Aduda kuwa Naibu Chansela mpya anayesimamia Fedha, Mipango na Maendeleo.

Baraza hilo pia lilimpongeza Margaret Jesang Hutchinson kwa huduma yake kama kaimu Naibu Chansela katika kipindi cha mpito, likisifu kujitolea kwake na uongozi wake.

Naibu Chansela huyo mpya sasa anaingia madarakani katika kipindi muhimu ambapo taasisi hiyo inakabiliwa na changamoto za kifedha pamoja na wasiwasi kuhusu usimamizi, wafanyakazi na masuala ya ustawi wa wanafunzi.

Uteuzi wa Ayub unakuja mwezi mmoja tu baada ya Chama cha wahadhiri na wafanyakazi wa vyuo vikuu nchini tawi la Chuo Kikuu cha Nairobi, kueleza wasiwasi kuhusu kuchelewa kwa uwepo wa uongozi wa kudumu katika taasisi hiyo.

Share This Article