Genge hatari la Nakuru lahusishwa na mauaji ya kasisi wa PCEA

Washukiwa wawili tayari wamefikishwa mahakamani kuhusiana na mauaji ya kasisi huyo yaliyotekelezwa Mei 4, 2026.

Tom Mathinji
1 Min Read
Genge hatari la Nakuru lahusishwa na mauaji ya kasisi wa PCEA.

Maafisa wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamehusisha mauaji ya Kasisi Julius Ndumia Ngari wa kanisa la PCEA na genge la wahalifu linalofahamika kwa wizi wa kimabavu katika kaunti ya Nakuru.

Maafisa wanaochunguza mauaji hayo yaliyowaacha wengi vinywa wazi, walisema genge hilo lilitambulika mara ya kwanza mwaka 2022 likijsingizia kuwa kundi la usalama lililokuwa na sare na ambalo lilitumia bunduki aina ya L1A1 kuwahangaisha wananchi.

Kupitia kwa taarifa, DCI ilihusisha genge hilo na wizi wa kimabavu usiku wa Mei 1,2026 ambapo shilingi 600,000 zilihamishwa kutoka akaunti ya benki ya mwathiriwa hadi kwa simu ambazo zilihusishwa na wanachama wa kundi hilo hatari.

Aidha, maafisa hao wanachunguza mienendo ya mashsambulizi katika kaunti ya Nakuru na viunga vyake, huku genge hilo likishukiwa kuhusika na visa hivyo.

“Uchunguzi wa kisayansi kuwahusisha washukiwa hao katika tukio la mkasa, bado unaendelea,” ilisema DCI.

Washukiwa wawili tayari wamefikishwa mahakamani kuhusiana na mauaji ya kasisi huyo yaliyotekelezwa Mei 4, 2026.

Washukiwa hao walipatikana na simu na kadi za simu za kasisi huyo.

Kasisi Ndumia alizikwa nyumbani kwake katika kaunti ya Nyeri Jumatatu Mei 11, 2026.

TAGGED:
Share This Article