Wilson Kigwa kupeperusha bendera ya Jubilee Ol Kalou

Kigwa alichaguliwa na chama hicho baada ya mashauriano na wadau na kutekeleza mchujo

Marion Bosire
1 Min Read

Mhandisi Wilson Kigwa ndiye mwaniaji wa chama cha Jubilee wa wadhifa wa ubunge katika eneo la Ol Kalou.

Kigwa alichaguliwa na chama hicho baada ya mashauriano na wadau na kutekeleza mchujo kwa ajili ya uchaguzi huo mdogo ujao.

“Chama cha Jubilee kimekamilisha rasmi mashauriano na mchakato wa mchujo, kwa ajili ya uchaguzi mdogo ujao wa ubunge katika eneo la Ol Kalou,” ilisema taarifa kutoka kwa uongozi wa chama cha Jubilee.

Kulingana na taarifa hiyo, mchakato huo mzima uliongozwa na katiba ya chama, bodi ya kitaifa ya uchaguzi, idara husika za chama na mashauriano na wawaniaji waliohitimu.

Wilson Kigwa atapambana na wawaniaji wengine kama Samuel Muchina Nyagah wa UDA na Sammy Ngotho wa DCP kwenye kinyang’anyoro hicho huku uchaguzi mdogo ukiandaliwa Julai 16, 2026.

Chama cha Jubilee kilisema kwamba marehemu mbunge wa Ol Kalou David Kiaraho, alichaguliwa kwa tiketi ya chama hicho na kimejitolea kuhakikisha kinadumisha urithi wake wa maendeleo na utoaji huduma huko.

Marehemu Kiaraho, aliaga dunia Jumapili Machi 29, 2026 akipokea matibabu katika hospitali moja ya Nairobi.

Share This Article