Mbwembwe za uapisho wa Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni kuhudumu kwa muhula wa saba ambapo chama tawala cha NRM kimepanga mengi ya kufana.
NRM inatarajiwa kuandaa maonyesho ya kuvutia ya droni na fataki usiku wa leo Jumatatu kuelekea kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni kesho.
Maonyesho hayo ya droni yatafanyika karibu na hoteli ya Protea jijini Kampala, ambapo droni zitarushwa angani na kuunda picha pamoja na jumbe mbalimbali.
Kwa mujibu wa Rosemary Sseninde, maonyesho hayo yataanza saa mbili unusu usiku na kudumu kwa takriban dakika 15 kabla ya kuhitimishwa kwa fataki.
“Yataonekana kutoka urefu wa mita 200 na ndani ya eneo la kilomita 3 hadi 5. Wale ambao hawatakuwa karibu wanaweza kufuatilia kupitia televisheni kwani vituo vingi vitaonyesha mubashara,” alisema Sseninde.
Aliongeza kuwa maonesho hayo yataangazia mafanikio muhimu ya Rais Museveni.
Wakazi wa maeneo yanayozunguka hoteli ya Protea, Kololo, Naguru, Nakasero na sehemu nyingine za katikati mwa Kampala wanatarajiwa kupata mwonekano mzuri zaidi wa maonyesho hayo.
Jayshree Suchak, anayejulikana pia kama Jay, alisema waandalizi wamefanya kazi kwa karibu na vyombo vya usalama kuhakikisha usalama wa tukio hilo.
“Kila mtu ataona jinsi picha hizo zitakavyojitokeza angani. Mtamuona rais akizungumza nanyi na kutakuwa na fataki baadaye; yatakuwa maonyesho ya dakika 15 yakionyesha sehemu tu ya mafanikio,” alisema Suchak.
Tukio hilo ni sehemu ya shughuli zinazoongoza kuelekea kwa kuapishwa kwa Museveni kunakotarajiwa kufanyika kesho Jumanne katika uwanja wa Kololo.
Usalama tayari umeimarishwa mjini Kampala kabla ya sherehe hizo, huku baadhi ya barabara zikitarajiwa kukumbwa na msongamano wa magari wakati wa maadhimisho hayo.