Baraza moja nchini Japan limepiga kura ya kumuondoa madarakani, meya wake ambaye amekuwa katika hali ya kupoteza fahamu kwa miezi kadhaa.
Kikuo Hatakeyama, mwenye umri wa miaka 72, amehudumu kama meya wa Hachirogata kaskazini mashariki mwa Japan tangu mwaka 2008, lakini aliugua mwezi Februari na kukumbwa na taizo la damu kuvuja kwenye ubongo.
Baraza la mji lilipitisha kwa kauli moja kura ya kutokuwa na imani na meya huyo, jambo ambalo linamaanisha atapoteza rasmi nafasi yake tarehe 19 Mei.
Chama cha kitaifa cha mabunge ya miji na vijiji nchini Japan kinasema ni nadra kwa kura ya kutokuwa na imani kuwasilishwa dhidi ya meya kutokana na ugonjwa.
Hoja hiyo ilisema kumuondoa Hatakeyama ni uamuzi mgumu, lakini muhimu kwa sababu za kiutawala.
Mke wake aliomba baraza la mji mwezi uliopita kutathmini kama angeweza kuendelea na wadhifa wake, akisema kuwa ingekuwa bora kwake kujiuzulu kama meya.
Sheria za eneo hilo zinawataka mameya wanaotaka kujiuzulu kulifahamisha baraza kupitia mwenyekiti wake.
Serikali ya mji ilisema mwezi uliopita kwamba ombi la kujiuzulu lililowasilishwa na watu wa familia ya Meya huyo, halingekuwa halali.
Kwa hiyo, kura ya kutokuwa na imani ilikubaliwa kama njia ya haraka zaidi ya kumuondoa meya huyo, huku uchaguzi wa kutafuta mrithi wake ukitarajiwa kufanyika ndani ya siku 50.