Sote Kama Familia kwa Pamoja kuafikia Azimio (Sofapaka FC ), ni klabu ya soka iliyobuniwa mwaka 2002, kutoka kwa kundi la ibada ya wanaume la kanisa la MAOS Kenya.
Klabu hiyo ilitwaliwa na mfanyabiashara wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Elly Mboni Kalekwa, mwaka 2004, ikidumisha jina SOFAPAKA.
Hata hivyo, kinyume na ilivyokuwa klabu hiyo ilisaini wachezaji kutoka nje ya kanisa la MAOS, na kufanikiwa kujiunga na ligi kuu taifa ukipenda Nationwide.
Miaka mitatu ikiwa bado chini ya umiliki wa Kalekwa,SOFAPAKA ukipenda Batoto ba Mungu, ilitwaa Kombe la Rais wakati huo ambalo kwa sasa linafahamika kama Mozzart Bet Cup.

Kunyakua Kombe hilo kuliwapa tiketi ya kuiwakilisha Kenya katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika, ila mvutano uliokuwepo wa usimamizi katika shirikisho la soka wakati huo ukawafanya Sofapaka kufungiwa nje.
Mwaka 2008 hatimaye timu hiyo ilitwaa ubingwa wa ligi ya Nationwide Zone B, na kupandishwa daraja kucheza Ligi Kuu mwaka 2009 na kunyakua taji ya ligi hiyo kwa mara ya kwanza.
Hata hivyo ,safari yao kushiriki Ligi ya mabingwa mwaka 2011 ilikuwa ngumu wakibanduliwa katika raundi ya mchujo na Ismailia ya Misri.
Mwaka 2010 timu hiyo ilishinda kombe la Rais kwa mara ya pili na kufuzu kwa Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2011, na kinyume na mara ya kwanza walicheza hadi ya raundi ya kwanza wakiibandua timu ya Atletico Aviacao ya Angola, katika raundi ya mchujo na kuibwaga Ismaily ya Misri katika raundi ya kwanza.

Katika raundi ya pili SOFAPAKA waliishinda St Eloi Lupopo ya Jamhuri ya Kidememokrasia ya Congo, lakini wakabanduliwa katika raundi ya tatu na Club African kutoka Tunisia, na kukosa fursa ya kucheza hatua ya makundi.
Batoto Ba Mungu, walirejea tena katika kombe la shiririsho waliponyakua Kombe la Rais kwa mara ya tatu mwaka 2015, ila wakayaaga mashindano katika hatua ya mchujo.
Hata hivyo safari yao katika Ligi ya Kenya ambayo ilifikia tamati wiki jana baada ya kutoka sare ya 2-2 na Mathare United, imekuwa na pandashuka zake.
Lakini historia kubwa ambayo klabu hiyo imeacha katika ligi ya Kenya ni kuleta kandarasi za wachezaji na pia ndiyo timu ya kwanza katika Ligi iliyowalipa wachezaji mishahara minono.

Kulingana na Rais Kalekwa, safari ya timu hiyo Ligini haijakuwa rahisi akitumia zaidi ya shilingi bilioni 1.1, kwa gharama ya kuendesha shughuli kwa kipindi cha miaka 17 ambayo wameshiriki ligi kuu.
Msimu wa mwaka 2025/2026 wa Ligi Kuu Kenya, umekuwa mgumu kwa SOFAPAKA, wakishinda mechi tatu pekee kati ya 30, walizopiga,wakitoka sare 9 na kupoteza 18.