Tiketi za tamasha ya mwanamuziki wa Rwanda King James ziliisha ndani ya muda wa siku tatu tu, baada ya mauzo kufunguliwa mtandaoni.
Nyingine zipatazo 1,400 zilikuwa zimeuzwa wakati wa mauzo ya awali hata kabla ya waandalizi wa tamasha hiyo kufungua rasmi mauzo ya tiketi zilizosalia Mei 2, 2026.
Tamasha hiyo inayoandaliwa na kampuni ya Intore Entertainment, ambayo imepatiwa jina la ’20 Years of King James’ inatarajiwa kuwa ya kipekee msanii huyo anapoadhimisha miaka 20 katika sanaa.
Mauzo hayo ya haraka ya tiketi ni ishara ya ushawishi wa kudumu alionao King James katika tasnia ya muziki pamoja na mtagusano wa kipekee na mashabiki wake.
Tamasha hiyo ya King James imepangiwa kuandaliwa katika ukumbi wa BK Arena jijini Kigali Agosti 1, 2026 na sasa waandalizi wanawaza kuandaa kwa siku mbili mfululizo kutokana na jinsi imepokelewa na umma.
King James ambaye jina lake halisi ni Ruhumuriza James, anatarajiwa kuandaa tumbuizo la kipekee siku hiyo. Alijiunga na tasnia ya muziki mwaka 2006 na safari yake katika muziki imekuwa nzuri.
Mashabiki wake waliokosa tiketi wamelalamika kwenye mitandao ya kijamii wakihimiza waandalizi kuongeza siku nyingine ya tamasha au kupanua eneo la maandalizi ili watu wengi zaidi wahudhurie.