Mwanamuziki wa Tanzania Christian Bella anapanga kuishukuru Tanzania kwa njia anayoifahamu vyema, muziki.
Msanii huyo ambaye ni mzaliwa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, amekuwa akiishi nchini Tanzania kwa muda sasa na ni huko ambako amejikuza kama mwanamuziki.
Ijumaa Mei 8, 2026, msanii huyo ameandaa tamasha kwa jina “Ahsante Tanzania” katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kwenye mahojiano, Bella alisema anaamini kwamba kila mmoja ana nyimbo angalau moja anayopenda kutoka kwake, ndiposa anaalika wote kwa tamasha hiyo.
“Njooni tusherehekee miaka 20 ya Christian Bella, tusherehekee kutoka mgeni na kuwa ndugu yenu, kwa hiyo ninawakaribisha watu wote,” alisema mwanamuziki huyo anayefahamika kwa mashairi yake matamu.
Kando na kuimba kama mwanamuziki huru, Bella amewahi kuimba pia kwenye bendi kama Chateau bendi na Malaika Band.