Uchunguzi wa maiti ya marehemu Daktari Job Obwaka umebainisha kwamba alifariki kutokana na mshtuko wa moyo.
Haya yalithibitishwa leo Jumanne Mei 5, 2026 na msemaji wa familia ya Daktari huyo aliyefariki ghafla akiwa na umri wa miaka 83. Kulingana na familia, Obwaka alikumbwa na mshtuko huo wa moyo, akapoteza fahamu na kisha kufariki.
Maafisa wa idara ya upelelezi wa jinai walisema kwamba huenda alitiliwa sumu katika makazi yanayoaminika kuwa ya mwanamke ambaye alikamatwa kwa kuhusishwa na kifo cha Obwaka.
Wachunguzi wanaamini mwanamke huyo alikuwa mtu wa mwisho kuonekana na daktari huyo kabla hajaanguka ghafla, imani iliyosababisha kukamatwa kwake mara moja.
Awali, upande wa mashtaka uliomba mahakama iwape wachunguzi siku 14 kukamilisha uchunguzi, ikiwa ni pamoja na uchunguzi wa maiti na uchambuzi wa sumu, lakini sasa majibu yametoka mapema.
“Kuna sampuli fulani zitakazowasilishwa kwa mchambuzi wa serikali, na huenda kutokana na vipimo au uchunguzi huo, pia kufanyike tathmini ya afya ya akili baadaye,” mwendesha mashtaka alisema.
Katika hati ya kiapo, afisa wa upelelezi alieleza kuwa sampuli zilizokusanywa kutoka makazi ya Wangari katika mtaa wa Milimani zitakuwa muhimu katika uchunguzi mzima kwa ajili ya vipimo vya kitaalamu vya kisayansi.
Dkt. Obwaka atakumbukwa kutokana na mvutano mkali wa uongozi ndani ya Chama cha Hospitali za Kenya kilicho na hisa katika umiliki wa Hospitali ya Nairobi.
Wiki chache kabla ya kifo chake mnamo Machi 2026, Dkt. Obwaka pamoja na wakurugenzi wengine watatu walikamatwa na kushtakiwa kwa mgongano wa maslahi, kushindwa kuwasilisha taarifa za kifedha kati ya mwaka 2022 na 2024, pamoja na kughushi kumbukumbu za wanachama.
Wakurugenzi hao walidai kukamatwa kwao kulikuwa vitendo vya unyanyasaji kutoka kwa “mawakala wa serikali” vilivyolenga kulazimisha kuchukuliwa kwa usimamizi.