Mshikilizi wa rekodi mpya ya Dunia ya marathon Sabastian Sawe, amelakiwa nyumbani katika kaunti ya Nandi siku Jumatatu kwa shangwe,vifijo na nderemo na Gavana Stephen Sang.
Hafla hiyo iliandaliwa katika uwanja wa michezo wa Eliud Kipchoge Complex.
Sherehe hiyo iliambatana na ibada ya maombi ya kutoa shukrani kwa ushindi wa Sawe, aliyeweka rekodi mpya ya marathon ya muda wa saa 1 dakika 59 na sekunde 30, aliposhinda London Marathon mwezi uliopita.
Sawe aliandamana na familia yake wakijumuisha mkewe, baba na mamake ,huku pia bingwa wa zamani wa Olimpiki Kipchoge Keino akihudhuria.
Gavana Sang amemtuza Sawe nyumba yenye vyumba vitatu ya kima cha shilingi milioni 4.8, na ng’ombe wa maziwa aina ya Freshian.
Nyumba hiyo iko chini ya nyumba za gharama nafuu eneo la Chesumei, mkabala na shule ya Kapsabet Boys.
Kaunti ya Nandi imemlaki Sawe siku kadhaa baada ya Rais William Ruto, kumpokea katia Ikulu ya Nairobi.