Mfumko wa bei waongezeka nchini Kenya

Marion Bosire
1 Min Read

Mfumuko wa bei wa kila mwaka nchini Kenya uliongezeka hadi asilimia 5.6 mwezi Aprili, kutoka kiwango cha awali cha asilimia 4.4 mwezi Machi, kulingana na Afisi ya Kitaifa ya Takwimu ya Kenya, KNBS.

Ongezeko hilo lilisababishwa na kupanda kwa bei za vyakula, usafiri na mafuta, kama ilivyoainishwa katika ripoti ya hivi karibuni ya Fahirisi ya Bei za Watumiaji.

Takwimu za KNBS zinaonyesha kuwa bei za vyakula na vinywaji visivyo vya kulewesha ziliongezeka kwa asilimia 8.8, gharama za usafiri zilipanda kwa asilimia 10, huku makazi, maji, umeme, gesi na mafuta mengine yakiongezeka kwa asilimia 2.4.

Mapema mwezi huo, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli, EPRA ilipandisha bei ya petroli ya super kwa shilingi 9.37 hadi Sh197.6 kwa lita, na dizeli kwa Sh10.21 hadi Sh196.63.

Mdhibiti huyo alieleza kuwa ongezeko la bei za mafuta lilitokana na kupanda kwa gharama za uagizaji wa mafuta duniani zinazohusishwa na usumbufu wa upatikanaji, licha ya kupunguzwa kwa ushuru ziada wa thamani wa mafuta kwa asilimia 8.

Share This Article