Kenya kunufaika kibiashara na soko la China

Tom Mathinji
1 Min Read

Kenya inatarajiwa kunufaika pakubwa na soko pana la China, huku bidhaa za Kilimo na zile zilizotayarishwa kuuzwa nje ya nchi, zikitarajiwa kuwa za ushindani mkali kwa mujibu wa balozi wa China nchini Kenya Guo Haiyan.

Guo alisema bidhaa kama vile Majani Chai, Kahawa, Maparachichi na bidhaa zilizotayarishwa ni miongoni mwa zile zinatarajiwa kufikia soko la China, chini ya mkakati huo mpya.

“Tunahimiza wafayabiashara kuchukua fursa hii. China imejitolea kufanya kazi kwa karibu na Kenya ili kuboresha ushirikiano dhabiti,” alidokeza Guo.

Alisema kuwa China kwa sasa haitozi ushuru bidhaa kutoka Mataifa 53 ya Afrika ambayo yana uhusiano wa kidiplomasia nayo, sera ambayo alisema ni ishara kuwa Beijing imejitolea kufungua ushirikiano ulio na manufaa.

“Uondoaji wa ushuru ni zaidi ya sera, ni kichocheo cha ukuaji wa viwanda, uongezaji thamani, na ubunifu wa nafasi za ajira na hivyo kuunga mkono ajenda ya maendeleo ya Kenya,” aliongeza balozi huyo.

Majadiliano kwenye mkutano huo yaliangazia ubora wa bidhaa, uidhinishaji na biashara za mipakani kidijitali ili kutoa uwezo kamili wa sera hiyo.

 

Share This Article