Taasisi ya Wangari Maathai ya mafunzo ya amani na mazingira, yaani “Wangari Maathai Institute (WMI)” imefunguliwa rasmi katika chuo kikuu cha Nairobi, bewa la Kabete ya juu.
Akizungumza wakati wa kuzindua rasmi taasisi hiyo, waziri wa mazingira Soipan Tuya aliwapa changamoto wakufunzi na wanafunzi wa taasisi hiyo wafanye utafiti na kuelezea kamili uhusiano uliopo kati ya mazingira, mizozo na amani.
Alisema serikali itashirikiana kwa karibu na taasisi ya Wangari Maathai kwenye mipango ambayo itasaidia Kenya na kanda nzima kukabiliana na changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi kama vile mizozo itokanayo na kung’ang’ania raslimali zinazopungua.
Waziri Tuya alisema kwamba ushahidi na takwimu vinaonyesha kwamba masuala ya mazingira na tabianchi yanachangia pakubwa ukosefu wa usalama, mizozo ndani ya nchi na kati ya nchi tofauti na bara Afrika limeathirika zaidi.
Alikuwa anamwakilisha Rais William Ruto kwenye uzinduzi huo ambapo alipongeza serikali na wadau wengine kwa kumkumbuka marehemu Maathai mshindi watuzo ya amani ya Nobel kupitia kufungua taasisi hiyo.
Taasisi hiyo ambayo ujenzi wake ulianza mwaka 2016, iliasisiwa na serikali kwa nia ya kuendeleza urithi wa Wangari Maathai na ilikabidhiwa chuo kikuu cha Nairobi mwaka 2019.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na uongozi wa chuo kikuu cha Nairobi wakiongozwa na Chansela Dr Vijoo Rattansi, kaimu naibu Chensela Profesa Julius Ogengo na mwenyekiti wa baraza la chuo hicho Profesa Amukowa Anangwe kati ya wengine wengi.