Washukiwa wakuu 12 wa ujambazi wakamatwa Nakuru

Tom Mathinji
1 Min Read
Washukiwa 12 wa uhalifu wakamatwa Nakuru.

Katika kile kinachoonekana kama juhudi za kukabiliana na visa vya ujambazi katika kaunti ya Nakuru, maafisa wa polisi wamewakamata washukiwa wakuu 12 wa uhalifu baada ya kutekeleza operesheni kali katika mtaa wa Kaloleni.

Baada ya kupokea habari za kijasusi, maafisa hao wa usalama walifanya msako kwenye maficho kadhaa ya washukiwa hao, ambapo walikamatwa walipokuwa wakipanga misururu ya uhalifu.

Kupitia ukurasa wa X, Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ilisema maafisa hao walipanua wigo wa msako wao hadi katika mtaa wa Freehold ambapo washukiwa  wanne walikamatwa.

“kwenye operesheni nyingine washukiwa wanane zaidi walikamatwa na hivyo kusambaratisha mtandao wa majamabazi ambao umewahangaisha wakazi wa Nakuru Mashariki na viunga vyake,” ilisema DCI.

Kulingana na idara hiyo, washukiwa hao wanazuiliwa katika korokoro za polisi wakisubiri kufikishwa mahakamani.

“Kupitia operesheni za kijasusi, Huduma ya Taifa ya Polisi imejitolea kuangamiza makundi yote ya majambazi kuhakikisha usalama kote nchini,” iliongeza idara hiyo.

TAGGED:
Share This Article