Mrembo Latricia Ian wa umri wa miaka 25, ndiye Miss World Tanzania mwaka 2026 kufuatia fainali ya mashindano hayo iliyoandaliwa jana usiku katika ukumbi wa Super Dome huko Masaki, jijini Dar es Salaam.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Muungano wa Tanzania, Gerson Msigwa alipatiwa jukumu la kutangaza mshindi jana usiku, huku mshikilizi wa taji ya Miss World Opal Suchaata na mwenzake wa Afrika Hasset Dereje Admassu nao wakijukumiwa kumvisha taji mshindi huyo.
Katika kiwango cha Tanzania, Latricia alikuwa anawakilisha eneo la Dar es salaam na sasa atawakilisha Tanzania katika awamu ya 75 ya mashindano ya Miss World kimataifa huko Vietnam mwezi Septemba mwaka huu.
Latricia amejikita katika kuunganisha urembo na dhamira ya Kijamii kupitia mradi wake wa Nuru ya Elimu unaolenga kuwezesha Vijana kupitia elimu.
Katika matokeo hayo, Nouru Masoud ni wa pili akifuatiwa na Paulina Allute, Silya Mussa na Dian Rutagalinda katika nafasi ya tatu, nne na tano mtawalia.
Kwa jumla washindani walikuwa 20 na kufikia usiku wa fainali hiyo jana, walikuwa wamesalia hao wa kwanza watano pekee.