Knockout ya Mama kuandaliwa mwezi huu

Tukio hilo litakutanisha mabondia wa ndani na nje ya Tanzania.

Marion Bosire
1 Min Read

Kampuni inayosimamia maandalizi ya michuano ya ndondi nchini Tanzania Mafia Boxing Promotion imetangaza rasmi ujio wa awamu ya nane ya mashindano ya ndondi ya Knockout ya Mama.

Kulingana na waandalizi mapambano hayo yatakuwa makubwa na yanatarajiwa kufanyika Aprili 24, 2026 katika Viwanja vya Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki, Ubungo, jijini Dar es salaam.

Mkurugenzi na Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Ally Zayumba, amesema tukio hilo litakuwa la kipekee likikutanisha Mabondia wa ndani na nje ya Tanzania, huku likilenga kuendeleza na kukuza tasnia ya ngumi nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Matangazo na Itifaki, Omary Clython, pambano hilo litakuwa na mvuto wa aina yake likijumuisha majina makubwa ya mabondia pamoja na pambano la marudiano kati ya Ibrahim Mafia na Alvin Camique kutoka Ufilipino.

Amesema pia kutakuwa na mapambano mbalimbali ya kimataifa yatakayowakutanisha Mabondia kutoka nchi tofauti, jambo linalotarajiwa kuongeza ushindani na burudani kwa mashabiki.

Aidha, usiku huo wa Knockout ya Mama, msimu wa nane, utapambwa na mapambano ya ubingwa yatakayohusisha mikanda minne ya kimataifa ya WBO katika uzani tofauti.

Share This Article