Jamaa mmoja aliyekuwa amejihami kwa bunduki wamewapiga risasi na kuwaua watoto wanane, saba kati yao wakiwa watoto wake, katika jimbo la kusini mwa Marekani la Louisiana.
Maafisa wa polisi wameripoti pia kumuua mtu huyo kwa kumpiga risasi.
Waathiriwa wa shambulio hilo, lililofanyika katika nyumba mbili huko Shreveport asubuhi ya Jumapili, walikuwa na umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi takriban miaka 12 kulingana na msemaji wa Idara ya Polisi ya Shreveport, Chris Bordelon.
Mmoja wa watu wazima waliojeruhiwa ni mama wa watoto wa mshukiwa.
Mshukiwa, ambaye Bordelon alimtambua kama Shamar Elkins, alifariki baada ya polisi kumkimbiza na kumpiga risasi alipokuwa akitoroka baada ya kuiba gari kwa kutumia bunduki.
Kiini cha vurugu hizo hakijabainika, Bordelon akisema bado kuna mengi ya kuchunguza, lakini wachunguzi wana uhakika kuwa ufyatuaji risasi huo ulikuwa tukio la kifamilia kabisa.
Bordelon alielezea kwamba Elkins alifahamika kwa polisi na alikamatwa mwaka 2019 katika kesi ya silaha. Maafisa hawakuwa na taarifa za matatizo mengine ya vurugu za kifamilia.
Meya wa Shreveport, Tom Arceneaux alitaja hali hiyo kuwa ya kusikitisha huku Spika wa bunge la wawakilishi la Marekani, Mike Johnson, ambaye ni mzaliwa wa Shreveport akisema anawasiliana na polisi wa eneo hilo kuhusu janga hilo la kuhuzunisha.
Gavana wa Louisiana, Jeff Landry na mke wake walidhihirisha huzuni kutokana na hali hiyo ya kutisha, na kwamba wanaombea kila aliyeathirika.
Bila kujumuisha kisa hiki cha Shreveport, shirika la kukadiria na kuweka kumbukumbu kuhusu vurugu za bunduki yaani “Gun Violence Archive” linaorodhesha matukio 119 ya ufyatuaji risasi kwa watu wengi nchini Marekani mwaka huu, yaliyosababisha vifo 117, wakiwemo watoto 79 huku watu 458 wakijeruhiwa.