Timu ya kina dada ya mchezo wa Voliboli ya DCI almaarufu DCI Queens imeingia kwenye robo fainali ya mashindano ya klabu bingwa cha voliboli barani Afrika baada ya kuishinda timu ya NAL ya Ethiopia.
Warembo hao wa DCI walikuwa na matokeo mazuri katika hatua ya makundi hali inayoaminika kuwamotisha kufanya vyema zaidi.
Mwanzo wa mchezo huo haukuwa rahisi kwani Queens walighubikwa na mashambulizi ya kasi ya juu na mpangilio wa haraka wa wapinzani wao huku NAL wakitangulia kudhibiti kasi ya mchezo na kuvuruga mpangilio wa Queens.
Licha ya juhudi za mwisho zilizosababisha Queens waokoe pointi mbili za seti, kosa la mwisho la kupasi mpira liliwapa NAL ushindi wa seti ya kwanza alama 26 kwa 24.
Hata hivyo, kushindwa huko kulichochea ari mpya baada ya Kocha Mkuu Patrick Sang pia kurekebisha kikosi chake.
Vizuizi vya ulinzi vilimarika, kupasi mpira kukawa kwa hali ya juu na kwa malengo zaidi, na ghafla mwelekeo wa mchezo ukabadilika.
Kutoka hali ya ushindani ya alama 11 kwa 12 katika seti ya pili, Queens walitanua pengo la pointi 7-2 lililobadili kabisa mkondo wa mchezo. Kilichofuata ni utawala kamili, huku DCI wakishinda seti hiyo kwa kishindo alama 25-12.
Katika seti ya tatu warembo hao waliongeza pengo hadi alama 25-13 na seti ya nne alama 25-16.
Kwa ushindi huo, sasa wanaingia robo fainali ambapo wanakutana na wapinzani wao wakubwa wa ndani, Kenya Pipeline katika pambano la kusisimua la Wakenya wote.