Rais William Ruto asema hatosikiliza wakosoaji

Alitangaza Kenya kuwa eneo la ujenzi na kwamba maendeleo ya miundombinu yanalenga kuhakikisha utoaji huduma kwa wote na katika kila eneo nchini.

Marion Bosire
1 Min Read

Rais William Ruto amesema hatapoteza muda kusikiliza wakosoaji bali atafanya kazi ya kuboresha viwango vya maisha ya Wakenya wote.

Kiongozi wa nchi alitangaza kwamba Kenya ni “eneo la ujenzi,” akiongeza kuwa maendeleo ya miundombinu yanayoendelea kote nchini yanalenga kuhakikisha utoaji wa huduma kwa wote na katika kila eneo la jamhuri.

Akizungumza alipohutubia waumini katika Kanisa la African Gospel Church huko Karen, Kaunti ya Nairobi baada ya ibada ya Jumapili, Kiongozi wa Taifa alisema kuwa maeneo ya mbali ya nchi kwa muda mrefu yamepuuzwa chini ya tawala zilizopita.

Rais aliambia wale wanaolinganisha Kenya na nchi nyingine katika eneo hili kwamba Kenya ni uchumi wa kipato cha kati, tofauti na nchi nyingine katika eneo hilo ambazo zimeainishwa kama Nchi Zenye Maendeleo Duni na ndiyo sababu gharama ya maisha nchini iko juu.

Baada ya ibada Rais William Ruto alizungumza na wananchi katika eneo bunge la Lang’ata kaunti ya Nairobi kabla ya kuelekea Italia kwa ziara rasmi.

Kulingana na msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, Rais William Ruto atakutana na mwenzake wa Italia Sergio Mattarella na waziri mkuu Giorgia Meloni anaposaka ufadhili wa miradi kadhaa yakiwemo mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Share This Article