Madereva wa Kenya huko DRC, watishia kugoma kufuatia kuuawa kwa mmoja wao

Dismas Otuke
1 Min Read

Madereva wa malori ya kubeba mizigo kutoka Kenya hadi Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wametishia kusitisha huduma kuingia nchini Congo, hadi pale haki itakapotekelezwa kwa mmoja wao aliyeuawa kikatili .

Madereva hao wameandamana siku ya Alhamisi wiki hii wakiitaka wizara ya mashauri ya kigeni ya Kenya,kuhakikisha usalama wa kutosha katika ushoroba wa mashariki kuingia nchini Congo.

Chama cha madereva na utingo wa magari ya usafiri wa mwendo mrefu ( LoDDCA), kimelalamikia kuzorota kwa hali ya usalama katika ushoroba wa mashariki mwa DRC.

LoDDCA imesikitishwa na kuuawa kwa dereva Edwin Njuguna, katika eneo la Bunia  mashariki mwa DRC kwa njia isiyoeleweka baada ya lori lake kuharibika likiwa njiani.

Chama hicho kimesema kitahiari kusitisha safari za kuingia DRC, endapo madereva hawatapewa hakikisho la usalama na serikali ya Kenya.

Aidha, familia ya mwendazake imeomba usaidizi wa kusafiri hadi DRC, ili kuusafirisha mwili wa mpendwa wao kwa  mazishi.

 

Share This Article