Usimamizi wa mashindano ya ulimbwende ya kitaifa nchini Tanzania almaarufu Miss Tanzania umebadilika.
Hatua hii ilijiri usiku wa jana Jumanne Aprili 14, 2025 huko Mlimani City jijini Dar es Salaam, katika hafla ambapo Mkurugenzi wa Kampuni ya The Look, Basila Mwanukuzi alikabidhi rasmi uendeshaji wa mashindano hayo kwa Leah Richard Mwendamseke.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wadau mbali mbali wa sekta ya burudani na urembo nchini Tanzania wakiwemo waigizaji na hata wadau wa kampuni ya sanaa na burudani ya Lamata anayomiliki Leah.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo Basila alisema kulikuwa na ushindani mkubwa wa kuwania nafasi hiyo, huku baadhi ya waliokuwa wakiimezea mate, wakitoka nje ya nchi wakiwa na nia ya kuendesha mashindano hayo ya ulimbwende.
Hata hivyo, alieleza kuwa aliridhishwa na uwezo wa Leah, akiamini ana sifa na maono ya kuipeleka Miss Tanzania katika kiwango cha juu zaidi.
Kwa upande wake, Leah alisema anashukuru kwa kuaminiwa na kupatiwa jukumu hilo muhimu, akiahidi kuendeleza ubunifu na ubora katika mashindano yajayo.
alisisitiza kwamba atalenga kufanya mabadiliko chanya yatakayovutia Washiriki wengi zaidi pamoja na kuinua hadhi ya mashindano hayo Kitaifa na Kimataifa.