Mahakama ya Rufani ya Tanzania, ambayo ni chombo cha juu zaidi cha utoaji wa haki nchini Tanzania, imefuta rasmi agizo lililotolewa awali la kuzuia chama cha upinzani CHADEMA kuhusika katika shughuli zozote za kisiasa.
Mahakama Kuu ya Tanzania ilikuwa imetoa agizo hilo kufuatia ombi lililowasilshwa na Saidi Issa na wenzake, waliokuwa wamefungua kesi inayohusu ugawaji wa mali za chama hicho.
Katika uamuzi wake, Mahakama ya Rufani imebainisha kuwa uamuzi uliokuwa umesababisha kusitishwa kwa shughuli za chama hicho haukuwa na misingi ya kutosha ya kuendelea kutumika, hivyo kuondoa vizuizi vyote vilivyokuwa vimewekwa.
Mahakama hiyo imesema, “Baada ya kupitia hoja zote zilizo mbele yetu, tumebaini kuwa hakuna sababu ya kisheria ya kuendeleza zuio dhidi ya chama husika, hivyo zuio hilo linafutwa mara moja na chama kinaruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kisiasa bila kikwazo.”
Chama cha Demokrasia na Maendeleo, CHADEMA kimekuwa kikipinga zuio hilo mara kwa mara kikisisitiza kwamba lilikuwa likisababisha athari kwa shughuli zake za ndani na za kisiasa, huku pia ikidai kuwa lilikuwa likitumiwa kama msingi wa kuvuruga mikutano yake.
Kwa kufutwa kwa zuio hilo, chama hicho sasa kimeruhusiwa rasmi kurejea katika shughuli zake zote za kisiasa nchini Tanzania.
Wadhamini watatu wa chama cha CHADEMA kutoka Zanzibar walikwenda mahakamani kutafuta maagizo ya kufungia mali za chama hicho pamoja na shughuli za kisiasa na walifanikiwa kupata maagizo hayo mwezi Juni mwaka 2025.
Watatu hao walilalamikia uwepo wa ubaguzi katika kugawa raslimali za chama hicho na kile walichokitaja kuuwa mzozo wa ndani kuhusiana na mali za chama.