Halmashauri ya kusimamia viwanja vya ndege nchini (KAA), imemteua Moses Wekesa kuwa Afisa Mkuu Mtendaji na Mkurugenzi Mkuu.
Huku ikitoa tangazo hilo, mwenyekiti wa bodi ya KAA Iltasayon Neepe, alisema Wekesa aliibuka bora kushikilia wadhifa huo na kupeleka mbele ajenda za halmashauri hiyo wakati wa mchakato wa kujaza nafasi hiyo.
Amachukua mahala pa Dkt. Mohamud Gedi ambaye alikuwa akikaimu wadhifa huo.
Wekesa ambaye awali alikuwa mfanyakazi wa KenGen, anatajiriba ya kuongoza miradi mikubwa katika masoko kadhaa barani Uropa,Pacific, Africa na Asia.
“Utaalam wake unajumuisha sekta ya miundombinu na kumpa fursa bora ya kuimarisha miundombinu katika sekta ya safari za ndege nchini,” ilisema taarifa ya KAA.
Wekesa amehitimu na shahada ya Uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) na shahada ya uzamili katika uhandisi wa kiufundi kutoka Chuo kikuu cha Nairobi.
Anatarajiwa kusaidia Halmashauri hiyo kutekeleza miradi muhimu ikiwa ni pamoja na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA).