Serikali kubadili eneo la Gusii kimaendeleo

Hayo ni kwa mujibu wa Rais William Ruto ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku nne katika eneo la Gusii.

Marion Bosire
1 Min Read

Serikali inapanga kubadilisha sura ya eneo la Gusii kwa kutekeleza miradi ya kimkakati katika kaunti ya Kisii na ile ya Nyamira.

Hayo ni kwa mujibu wa Rais William Ruto ambaye yuko katika ziara ya kikazi ya siku nne katika eneo la Gusii ambapo alisema pia kwamba wanashirikiana na viongozi kuhakikisha hakuna eneo linasalia nyuma kimaendeleo.

Akizungumza katika mkutano aliofanya na viongozi waliochaguliwa wa eneo la Gusii katika Ikulu ndogo ya Kisii, Rais alisema miradi iliyopatiwa kipaumbele ni pamoja na nyumba za gharama nafuu.

Miradi mingine aliyotaja ni pamoja na masoko ya kisasa, nyumba za makazi kwa wanafunzi, barabara na madaraja, viwanja vya michezo na miradi ya maji, miongoni mwa miradi mingine ya maendeleo ya miundombinu, ili kufungua uwezo wa kiuchumi wa eneo hilo na kuinua jamii kutoka chini.

Matokeo ya uwekezaji huo kulingana na kiongozi wa nchi, yanajieleza yenyewe katika kaunti hizi mbili.

Viongozi wa Kisii na Nyamira waliohudhuria mkutano wa jana jioni ni Magavana Simba Arati wa Kisii na Amos Nyaribo wa Nyamira, wabunge na wawakilishi wadi.

Walihadili kuhusu vipaumbele vya maendeleo katika eneo hilo, wakihakikisha mipango yao inaambatana na mahitaji ya watu.

Share This Article