Seneti yaombwa kuharakisha ripoti kuhusu kufanya mji wa Thika kuwa jiji

Wito huu ulitolewa katika kikao cha kuhusisha umma cha kujadili suala hilo la hadhi ya jiji.

Marion Bosire
1 Min Read
Kimani Wamatangi, Gavana, Kiambu, akihutubia kikao cha kujadili hadhi ya jiji kwa manispaa ya Thika.

Viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Kiambu na jamii ya wafanyabiashara mjini Thika, wameomba bunge la Seneti liharakishe kuandaa na kukamilisha ripoti itakayowezesha mji wa Thika kupatiwa hadhi ya jiji.

Wito huu ulitolewa katika kikao cha kuhusisha umma cha kujadili suala hilo la hadhi ya jiji pamoja na wanachama wa kamati ya bunge la Seneti kuhusu ugatuzi na uhusiano kati ya serikali kuu na serikali za kaunti.

Gavana wa kaunti hiyo ya Kiambu Kimani Wamatangi aliwasilisha rasmi ombi la kubadili mji wa Thika kuwa jiji kwa kamati hiyo, ndiposa ikaamua kufika nyanjani kupokea maoni ya wakazi.

Wanabiashara wanaotekeleza shughuli zao mjini Thika wakiwemo waendeshaji boda boda walikubaliana kwa kauli moja kwamba kupandishwa hadhi kwa mji huo kutaimarisha uchumi.

Viongozi wa eneo hilo waliokuwepo nao waliunga mkono pendekezo hilo lakini wakaonya kwamba mabadiliko hayo hayafai kuvuruga shughuli za biashara kwa vyovyote.

Gavana Wamatangi alihakikishia wanabiashara kwamba maslahi yao yatalindwa kikamilifu wakati ambapo kamati hiyo ya Seneti inatarajiwa kuwasilisha ripoti kuhusu suala hilo bungeni wiki ijayo ili iangaziwe.

Share This Article