Serikali imemakinika kuboresha maisha ya Wakenya, asema Rais Ruto

Tom Mathinji
2 Min Read

Rais William Ruto alishiriki meza ya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Mlima Kenya na kitui siku ya Jumanne.

Kwenye mkutano huo ulioandaliwa katika Ikulu ya Nairobi, kiongozi wa taifa alisema walikubaliana kuharakisha miradi ya maendeleo ili kutoa fursa zaidi, kuimarisha biashara katika maeneo hayo na kuboresha maisha ya wakazi.

Kupitia kwa taarifa kwenye ukurasa wake wa X,  Rais Ruto alidokeza kuwa  serikali inajizatiti kubadilisha sura ya kaunti ya Nyeri kupitia miradi ya miundombinu ikiwa ni pamoja na kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara ya safu mbili ya Kenol-Karatina-Marua.

” Tunabadilisha sura ya kaunti ya Nyeri kupitia miradi ya maendeleo ya miundombinu,” alisema Rais Ruto.

Miradi mingine aliyosema serikali inatekeleza ni pamoja na ujenzi wa nyumba 8,000 za gharama nafuu, masoko 20 ya kisasa na nyumba za malazi kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na taasisi zingine za elimu ya juu pamoja na kuimarishwa kwa uwanja wa Ruring’u.

Kuhusu kaunti ya kitui, viongozi walijadili miradi ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kukamilishwa kwa ujenzi wa bwawa la Thwake na uchimbaji visima vya maji.

Miradi iliyoangaziwa Murang’a ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Mau Mau, viwanja vya michezo vya Mumbi na Gakoigo, hospitali ya Kenneth Matiba, mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na uunganishwaji wa stima.

Share This Article