Mapato kutokana na mauzo ya Majani Chai nje ya nchi,yameongezeka hadi shilingi bilioni 186.9, hatua ambayo imesababishwa na ongezeko la hitaji la bidhaa hiyo katika soko la kimataifa.
Takwimu za hivi punde kutoka Bodi ya Majani Chai ya Kenya (TBK), zinaonyesha kuwa mapato kutokana na mauzo ya bidhaa hiyo mwaka jana yaliongezeka kwa asilimia 2.9 kutoka shilingi bilioni 181.7 mwaka 2024.
Katika kipindi hicho, TBK ilisema kuwa kiwango cha mauzo nje ya nchi kiliongezeka kwa asilimia 9.8, hii ikiwa sawa na kilo milioni 58.3.
Akizungumza wakati wa kutangazwa kwa takwimu hizo, Waziri wa Kilimo na Ustawi wa Mifugo Mutahi Kagwe, alisema licha ya changamoto zilizoshuhudiwa mwaka uliopita ikiwa ni pamoja na ubadilishanji wa fedha za kigeni, mizozo katika baadhi ya masoko na ukuaji hafifu wa uchumi wa dunia, sekta hiyo ilisalia imara.
“Mnamo mwaka 2025, thamani ya soko ya Majani Chai ya Kenya ilifika shilingi bilioni 218.79, hii ikiwa ni ongezeko ya asilimia mbili kutoka thamani ya shilingi billioni215.21 mwaka 2024,” alisema Kagwe.
Aidha kulingana na TBK, bei ya mauzo ya nje ya nchi ilitatizwa na ubadilishanaji wa sarafu ya dola ya Marekani.